Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Dkt. Yusuph Mashala, jana tarehe 17 Julai, 2025 amepokea ugeni kutoka kwa Ofisa wa Polisi wa Wilaya ya Mtumba, ASP Charles Mwamtobe, aliyeambatana na Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Hombolo, Inspekta Mlangila. Ziara hiyo ililenga kujitambulisha rasmi kwa uongozi wa chuo pamoja na kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na Chuo cha Serikali za Mitaa, hasa katika maeneo ya ulinzi na usalama wa jamii.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Chuo, viongozi hao walijadiliana kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa mahusiano imara na ya karibu kati ya Jeshi la Polisi na jumuiya ya Chuo cha Serikali za Mitaa ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa katika eneo la Hombolo na maeneo jirani.
ASP Mwamtobe alieleza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kutoa ushirikiano wa karibu kwa taasisi zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Mtumba, ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu ya juu kama Chuo cha Serikali za Mitaa, kwa kuhakikisha mazingira salama ya kujifunzia, kufanyia kazi na kuishi kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo.
Kwa upande wake, Dkt. Mashala aliwashukuru maofisa hao kwa ziara yao ya heshima na kuonyesha utayari wa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha usalama wa jamii. Aidha, alisisitiza kuwa chuo kinaweka kipaumbele katika usalama wa wanafunzi, watumishi na majirani wa chuo, hivyo uwepo wa ushirikiano na Jeshi la Polisi ni jambo la msingi na la kupongezwa.
Ziara hiyo imeweka msingi mzuri wa mahusiano kati ya Chuo cha Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi, ikiwa ni hatua muhimu ya kuelekea katika kujenga jamii yenye usalama, utulivu na mshikamano.