KIGOMA:
Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) kimefunga rasmi mafunzo kwa madiwani kutoka halmashauri zote 184 nchini, yaliyokuwa yakitolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao wapya waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akifunga mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale, , aliwapongeza madiwani kwa kuchaguliwa na wananchi na kuwataka kuyatumia mafunzo hayo ipasavyo ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kata wanazoziongoza.
Alisema kuwa hatua ya kuwapatia mafunzo madiwani kabla ya kuanza rasmi kwa vikao vya mabaraza ya madiwani inalenga kuwajengea uelewa sahihi wa majukumu yao na hivyo kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Mafunzo hayo yalianza Desemba 15, 2025 katika mkoa wa Geita na kufanyika katika halmashauri zote 184 nchini, huku mkoa wa Kigoma ukipewa heshima ya kuwa mwenyeji wa hafla ya kufunga mafunzo hayo kitaifa.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Dkt. Mashalla Yusuph Lameck aliwahimiza madiwani kuhamasisha wanafunzi waliohitimu kidato cha nne pamoja na wazazi wao kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya kujiendeleza kielimu.
Alieleza kuwa chuo hicho kina kampasi mbili katika mkoa wa Dodoma, ambazo ni Hombolo na Dodoma Mjini, na hivi sasa kimeanzisha kampasi mpya katika mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kozi za Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma) na Shahada (Degree).
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri, Profesa Magreth Bushesha alisema mafunzo hayo yalijikita katika mada mbalimbali muhimu ikiwemo uongozi na utawala bora, sheria za uendeshaji wa serikali za mitaa, muundo na majukumu ya diwani, uendeshaji wa mikutano, usimamizi wa watumishi, uandaaji wa bajeti na usimamizi wa mapato na matumizi.
Mada nyingine zilihusu usimamizi wa miradi ya maendeleo, usimamizi wa rasilimali ardhi, maadili ya madiwani pamoja na haki na stahiki zao.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma, Mganwa Nzota alisema ni heshima kubwa kwa mkoa huo kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa hafla ya kufunga mafunzo hayo kitaifa baada ya wakufunzi kutembelea halmashauri zote nane za mkoa huo.
Naye Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mussa Maulidi Ibrahim aliiomba serikali kupitia TAMISEMI kuendelea kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa madiwani ili kuongeza uwezo wao wa kuziendesha halmashauri kwa ufanisi.
Aidha aliwataka madiwani kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri na kuepuka migogoro isiyo na tija ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya jitihada za Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) katika kuimarisha uongozi na utendaji wa serikali za mitaa nchini.